Kwa mashabiki wa Simba mitaani na mitandaoni, matumaini ni makubwa kuelekea msimu mpya wa mashindano. Uongozi mpya umeonyesha dhamira ya kujenga kikosi kipya kitakachojipambanua kwa ubora, huku kocha Fadlu Davids akibeba jukumu kubwa la kuliongoza benchi la ufundi.
Safari ya Fadlu
Tangu ajiunge na Simba Julai 5, 2024, Davids ameiongoza timu katika mechi 427. Alichukua nafasi iliyoachwa na Abdelhak Benchikha na hadi sasa ameiwezesha Simba kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika. Ingawa walishindwa kutwaa taji hilo, safari hiyo ilionyesha uwepo wa mwanga mpya chini yake.
“…Simba ni timu ya mataji, kwa hiyo muhimu kwake ni kuhakikisha wanabeba ubingwa…”
Mohamed Badru, Mchezaji wa zamani simba
Kikosi chake pia kimeendelea kujipanga, japokuwa changamoto za kufungwa na timu kama RS Berkane na Wydad Casablanca bado zinabaki kumbukumbu. Licha ya changamoto hizo, mashabiki wanatambua mchango wake katika kuibadilisha Simba.
Rekodi na Historia
Kwa upande wa makocha waliowahi kuinoa Simba, Patrick Aussems anaendelea kushikilia rekodi ya kudumu muda mrefu zaidi ndani ya klabu hiyo (siku 499). Kocha huyo aliwapa Simba mafanikio makubwa, ikiwemo taji la Ligi Kuu Bara msimu wa 2018/19 na kufika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Ikumbukwe, Aussems aliachwa baada ya msimu wa 2019/20 licha ya kuonyesha uimara. Hii inaonyesha ugumu wa kudumu ndani ya Simba, klabu yenye matarajio makubwa kila msimu.
Mitazamo ya Wachambuzi;
- Wachambuzi wa soka nchini wameeleza kuwa jambo muhimu kwa Fadlu Davids ni kuhakikisha Simba inatwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara na kuendelea kuwa tishio kwenye michuano ya kimataifa.
- Mohamed Badru, mchezaji wa zamani wa Simba, alisema:
“Amefanya kazi nzuri katika msimu wake wa kwanza. Simba ni timu ya mataji, kwa hiyo muhimu kwake ni kuhakikisha wanabeba ubingwa.” - Creed Mwaipopo, mchezaji wa zamani wa Yanga, aliongeza:
“Hakuna kingine kinachoweza kumfanya kocha akakaa muda mrefu isipokuwa matokeo. Ulaya wanaweza kumpa muda kocha ajenge timu, lakini Afrika matokeo ni kila kitu.”


